Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Dkt. Hussein Mohamed Omari ameitaka Bodi ya KoroshoTanzania kukaribisha wawekezaji katika kongani la viwanda lililopo katika Kijiji cha Maranje Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara ikiwa ni Pamoja na kuhakikisha kuwa mkandarasi anamaliza kazi yake kwa wakati stahiki kwani agenda ya serikali ni kuwa ifikapo 2030 korosho yote inayozalishwa nchini Tanzania iweze kubanguliwa.
Dkt. Hussein ameyasema hayo Februari 23, 2025 alipotembelea mradi huo wenye ukubwa wa hekari 1572 na kuongeza kuwa Wizara ya Kilimo imeandaa mpango kabambe wa mageuzi ya kilimo ya kutoka 2025 mpaka 2050 ambao umeainisha mazao ya kipaumbele 15 na miongoni mwa mazao hayo ni Korosho na Ufuta.
Naye Kaimu Meneja wa Ubanguaji wa Bodi ya Korosho ndg. Mangile Malegesi wakati akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa viwanda hivyo kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo amesema kuwa mradi huo utakwenda kuleta mabadiliko makubwa kwa kuzalisha ajira zaidi ya elfu 35 na kuongeza mapato serikalini.
Mradi huu ni maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa mwezi septemba 2023 akiwa katika ziara yake katika mikoa ya Lindi na Mtwara ambapo alitoa maelekezo ya kuanzisha kongani la viwanda kwa ajili ya kusindika mazao mengine ikiwamo ufuta ili kuyaongezea thamani.
Hivyo Bodi ya Korosho Tanzania ilipokea maelekezo kutoka Wizara ya Kilimo ya kutafuta eneo kwa ajili ya kuanzisha mradi huu katika Kijiji cha Maranje Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara.