Machi 26, 2025 07:41
Bodi ya Korosho Tanzania
Habari ZinazojiriKiteleziMatukio

UBALOZI WA TANZANIA-UAE, CBT WAPANGA MIKAKATI KULITUMIA SOKO LA KOROSHO NCHI ZA GHUBA KUPITIA UAE

Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho Tanzania wamepanga mikakati ya kulitumia ipasavyo soko la Korosho la Nchi za Ghuba kupitia Dubai, ambalo ndio kitovu cha biashara katika ukanda huo.

Hayo yamebainishwa wakati wa kikao kati ya Ubalozi na Ujumbe wa Tanzania uliotembelea Ubalozi huo tarehe 24 Februari, 2025      katika kikao maalum cha kupanga mkakati huo.

Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania Ndg. Francis Alfred akiambatana na Mkurugenzi wa Masoko na Udhibiti Ubora pamoja na Meneja Tawi la Morogoro, wengine ni wajumbe kutoka Taasi ya Utafiti ya Kilimo Tanzania (TARI), Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Chama Kikuu cha ushirika cha MAMCU na TCCIA.

Tanzania ni nchi ya pili Afrika kuzalisha Korosho pia ni nchi ya tano Duniani, katika msimu wa mwaka 2024/2025 uzalishaji umefikia zaidi ya tani 528,000 na Katika mkutano huo, Korosho ya Tanzania ilielezwa kuwa ni miongoni mwa korosho bora duniani kutokana na vigezo vya korosho vya soko la kimataifa duniani vikiwemo rangi nyeupe, ukubwa wake na ladha nzuri.

Katika Mkutano wa Dunia wa Korosho uliofanyika Dubai kuanzia tarehe 21 hadi 23 Februari 2025, Tanzania ilifanya vyema kwa kuwa na banda la maonesho ili kuitangaza Korosho, fursa za uwekezaji na kongani la viwanda maranje ambapo Kila mshiriki alipata fursa ya kuelimishwa kuhusu maendeleo ya Tasnia ya Korosho nchini Tanzania na kwamba nchi ipo tayari kutoa vivutio kwa wawekezaji watakaokuwa tayari kuja kuwekeza katika zao la Korosho kwa kufuata mnyororo wa thamani!

Aidha, UAE ilifahamishwa kuwa tayari Bodi ya Korosho Tanzania kwa kushirikiana na wizara ya Kilimo, imetenga eneo la kongani la viwanda inayojengwa katika kijiji cha Maranje Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara lenye jumla ya hekari 1,572, likitarajiwa kuwa na viwanda zaidi ya 60 ambalo litagharimu takribani Sh. bilioni 5.6 na kutoa ajira za kudumu 35,000.

Related posts

UZINDUZI WA BARAZA LA WAFANYAKAZI

Fesam

MATUMINZI YA SERIKALI MTANDAO KATIKA UTUNZAJI NYARAKA

Peter Luambano

BODI YA KOROSHO YAZINDUA RASMI MKUTANO WA KIMATAIFA WA KOROSHO 11-13 OCTOBA 2023 JNICC-DAR ES SALAAM

Peter Luambano