Machi 26, 2025 06:50
Bodi ya Korosho Tanzania
Habari ZinazojiriKiteleziMatukio

MKUU WA WILAYA YA TANDAHIMBA AMEZINDUA UGAWAJI PIKIPIKI NA VISHIKWAMBI KWA MAAFISA KILIMO WA BBT-KOROSHO

Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba Mhe. Kanali Michael Mtenjele, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Kanali Patrick Sawala, amezindua ugawaji pikipiki 500 na vishikwambi 500 kwa Maafisa kilimo wa BBT- Korosho huku akiwataka kufanya kazi kwa bidii, weledi na uwajibikaji ili kuleta mabadiliko Chanya katika tasnia ya Korosho.

Kanali Mtenjele amewataka vijana hao kuzitumia pikipiki hizo kwa ufanisi mkubwa ili kuuwezesha mkoa kufikia tani 420,400 za korosho ghafi zitakazochangia kwenye malengo ya uzalishaji ya jumla ya tani 700,000 kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania ndg. Francis Alfred amesema kuwa hatua hii ni utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa kwa Waziri wa kilimo Mhe. Hussein Bashe ikiwa ni jitihada za kuendelea kuongeza mchango wa zao hili katika kuongeza kipato kwa wananchi na pato la Taifa kwa ujumla.

Pia Mkurugenzi Mkuu ameeleza kuwa ili kufikia lengo la kuongeza uzalishaji wa korosho kutoka Tani 528,262.23 msimu wa 2024/25 hadi kufikia tani 700,000 msimu wa 2025/26 na tani 1,000,000 ifikapo 2030 ikiwa ni jitihada za kuongeza mchango wa zao la korosho kufikia agenda 10/30; serikali imeamua kuajiri vijana 500 wa BBT ambao tayari wamesambazwa katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani na Tanga.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Bodi ya Korosho Tanzania Brg Gen Aloyce Mwanjile ndc, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada zake za kuiwezesha Bodi ya Korosho Tanzania kutimiza malengo iliyopewa. Rais Dkt. Samia ametoa Pembejeo bure zilizosaidia kuongeza uzalishaji na kuimarisha bei ya Korosho. Pia Brig Gen Mwanjile ndc, amemshukuru waziri wa kilimo Mhe. Hussein Bashe kwa miongozo anayoitoa katika kuhakikisha malengo yaliyowekwa kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yanafikiwa.

Uzinduzi huo umefanyika katika ofisi za Bodi ya Korosho Tanzania manispaa ya Mtwara Mikindani Mkoani Mtwara machi 10, 2025 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mtwara, wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wa Halmashauri, Mkurugenzi wa kituo cha utafiti TARI Naliendele, mwakilishi wa Katibu Mkuu wizara ya Kilimo, Vijana wa BBT- Korosho, Wanahabari pia Menejimenti na watumishi wa Bodi ya Korosho Tanzania.

Related posts

DKT. SERERA AONGOZA KIKAO NOVEMBA 13-2024

Amani Ngoleligwe

TASNIA YA KOROSHO YAZIDI KUCHANGIA UCHUMI NCHINI

Amani Ngoleligwe

Bodi ya Korosho yawaonya wafanyabiashara wanaozitorosha Korosho nje ya nchi

Peter Luambano