Meli iliyobeba zaidi ya tani 9202 kati ya tani zaidi ya 40,000 za salfa zinazotarajiwa kuwafikia wakulima wa korosho katika msimu wa 2025/26 imewasili katika bandari ya Mtwara ikitokea nchini Uturuki.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania ndg. Francis Alfred alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari katika Bandari ya Mtwara, ambapo ameeleza kuwa katika msimu wa mwaka 2025/2026 hadi kufikia mwezi Mei, 2025 kutakuwa na zaidi ya tani elfu hamsini ikijumuisha bakaa ya tani elfu kumi zilizobaki katika msimu wa 2024/2025. Alieleza kuwa pembejeo hizo zitasambazwa kwa wakulima mapema ili ziweze kuwafikia kwa wakati.
Vilevile Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho amewasihi wakulima wote wa zao la korosho kuhakikisha kuwa wanahuisha taarifa zao kwa maafisa kilimo walioajiriwa chini ya mpango wa Jenga Kesho Iliyo Bora (Building a Better Tomorrow – BBT) kupitia ofisi za watendaji wa vijiji yalipo mashamba yao ili waweze kunufaika na pembejeo hizo zinazotolewa bure na Serikali.
Kwa upande wake Meneja wa Bandari ya Mtwara, Bw. Ferdinand Nyathi, amesema kuwa Bandari hiyo inaendelea kuhudumia meli zinazobeba viuatilifu vya zao la korosho huku akiongeza kuwa Bandari hiyo imejipanga katika kuhakikisha usalama wa pembejeo hizo na maandalizi mengine muhimu kuhakikisha kwamba ushushaji wa pembejeo hizo unafanyika kwa ufanisi tayari kwa kusambazwa kwenda kwa wakulima.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, Kanali Michael Mtenjele amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa kipaumbele wakulima wa zao la Korosho, na kueleza kwamba Serikali ya Mkoa itaendelea kuiunga mkono bandari ya Mtwara katika kuhakikisha majukumu yao yanafanyika kwa utaratibu unaotakiwa.