Bodi ya Korosho Tanzania (Bodi) ni taasisi ya Umma iliyopewa jukumu la kudhibiti
na kusimamia tasnia ya korosho nchini kuanzia uzalishaji, uongezaji wa thamani
pamoja na masoko. Aidha sheria ya Tasnia ya Korosho imeruhusu Bodi kuratibu na
kusimamia shughuli za kilimo, uwekezaji, Biashara na miradi ya maendeleo yenye
manufaa katika ustawi wa tasnia ya korosho. Hivyo Bodi inapenda kutangaza fursa
za uwekezaji kwa njia ya ubia zilizopo kwenye tasnia ya korosho. Aidha, Uwekezaji
huo utafanyika kwa kuzingatia sheria ya tasnia pamoja na miongozo na sera ya
Uwekezaji ya Ubia inayoratibwa chini ya Bodi.
- Fursa zinazotangazwa ni kama ifuatavyo:
i. Uwepo wa maeneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya uongezaji wa thamani
wa zao la korosho katika Kongani la viwanda lililopo kijiji cha Maranje, Kata
ya Mtiniko Halmashauri ya Nanyamba katika Mkoa wa Mtwara. lengo la
uanzishwaji wa kongani hili la viwanda ni kutekeleza malengo ya Serikali ya
kubangua korosho zote zinazozalishwa hapa nchini ifikapo mwaka 2030.
Kongani hilo la Viwanda lina ekari 1,572 ambapo eneo la ekari 354 tayari
limeshaandaliwa kwa shughuli za uwekezaji na lina miundombinu muhimu
kiwemo barabara, umeme, maji nk,
ii. Uwepo wa Viwanja viwili Mkoani Mtwara vilivyopo jirani na ufukwe wa Bahari
ya Hindi (Beach plots) kwa ajili ya ujenzi wa ghala au kiwanda; Maeneo haya
yapo mkabala na bandari ya Mtwara. Hivyo ni maeneo ya kimkakati kwa
uwekezaji wa ghala kwa ajili ya hifadhi ya mazao, pembejeo na shughuli za
viwanda. Aidha, yapo maeneo mengine yanayofaa kwa shughuli za makazi
na biashara.
iii. Uwepo wa maeneo kwa ajili ya uanzishaji wa mashamba makubwa ya
pamoja (block farms) katika mikoa ya Pwani, Lindi na Mbeya.
iv. Aidha, Bodi inayo maeneo katika jiji la Dar es Salaam yanayofaa kwa ujenzi
wa ofisi na shughuli za uzalishaji mali. - Vigezo vya kuwekeza katika maeneo ya ubia na Bodi ya;
i. Kurejea tangazo la Bodi la maeneo yanayotarajiwa kuendelezwa kwa njia
ya ubia.
ii. Muombaji kuwasilisha pendekezo la mradi anaotarajia kuwekeza katika
eneo husika, akieleza aina ya mradi tarajiwa, rasimu ya michoro, wigo wa
mradi, makadirio ya gharama, mipango ya utekelezaji na gharama,
uendeshaji na mapato tarajiwa;
iii. Mwombaji atawasilisha nyaraka za usajili wa kampuni yake inayoomba
kuwekeza kwa njia ya ubia;
iv. Bodi itajiridhisha kwa kufanya upekuzi unaostahili (due diligence) kwa
muombaji ili kubaini hali yake ya kisheria, ustadi wa kiufundi, uwezo wa
kifedha na taarifa nyingine zozote muhimu zinazohusiana na uwezo wake
wa kutekeleza kikamilifu mradi unaopendekezwa;
v. Bodi itapitia nyaraka za miradi zilizowasilishwa na kufanya maamuzi
kulingana na sera yake ya uwekezaji katika miradi ya ubia;
vi. Bodi itaingia mikataba ya ubia na makampuni au taasisi zilizosajiliwa kwa
mujibu wa sheria za Tanzania; na
vii. Mwekezaji atatakiwa kuweka Dhamana ya Uendelezaji (Development
Bond) baada ya kusaini mkataba kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi
kwa mujibu wa makubaliano yatakayofikiwa.