Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania ndg. Francis Alfred amekabidhi mashine nne za kubangulia korosho kwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mtwara Mhe. Shadida Ndile na diwani wa viti maalum Mhe. Zuhura Mikidadi ikiwa ni sehemu ya kuongeza jitihada za kukuza ubanguaji wa korosho nchini kwa wajasiriamali.
Ndg. Alfred amesema kuwa moja ya jukumu la bodi ya korosho ni kuisaidia jamii katika kuipatia vitendea kazi, pia amemtaka mstahiki meya kuijulisha bodi ya korosho endapo kutakuwa na uhitaji zaidi ambapo utaandaliwa utaratibu maalum wa kupatiwa mashine hizo kwani pia Bodi ya Korosho inatekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ubanguaji wa korosho nchini Tanzania ni sehemu muhimu katika sekta ya kilimo inayochangia kuongeza thamani ya zao la korosho, na kutokana na uhalisia kuwa Tanzania huzalisha korosho zenye ubora wa hali ya juu, serikali imewekeza katika ujenzi wa viwanda vya ubanguaji, lengo likiwa ni kuongeza thamani ndani ya nchi na kupanua ajira, hasa kwa vijana na wanawake.
Kwa miaka ya hivi karibuni, juhudi zimeongezeka kupitia ushirikiano wa Serikali pia Bodi ya Korosho Tanzania na Kwa kuongeza uzalishaji wa korosho zilizobanguliwa, Tanzania inalenga kuongeza mapato ya wakulima, kupanua masoko ya nje, na kushindana katika soko la kimataifa la bidhaa zilizoongezwa thamani.