Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania CBT) Ndg. Francis Alfred amesema kuwa hali ya soko la korosho ndani na nje ya nchi iko vizuri na kuwataka wakulima na wadau wengine kwenye mnyonyoro wa thamani kuendelea kusimamia na kuhakikisha korosho zinazopelekwa sokoni zina ubora unaokidhi vigezo vyote katika soko la Dunia.
Ndg. Alfred ameyasema hayo oktoba 19, 2024 wakati akifungua mnada wa Chama Kikuu Cha Ushirika Cha Lindi Mwambao, ambao umefanyika katika kijiji Cha Tulieni Mkoani Lindi.
“Hali ya soko mwaka huu imekaa vizuri, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amepambana kutafuta masoko kwa ajili ya mazao ya biashara nchini hasa kwenye zao la korosho,” amesema.
Amesema ubora wa korosho utasaidia kuhakikisha bei inaendelea kuwa nzuri kwa muda mrefu.
Ameongeza kuwa uwekezaji mzuri uliofanywa na serikali ya awamu ya sita ikiwa ni pamoja na kutoa pembejeo buree kwa asilimia mia na kwa wakati umesaidia kuongeza uzalishaji na ubora wa korosho.
Sambamba na hayo amewataka wakulima kuendelea kuyatunza mashamba yao ikiwa ni pamoja na kuyafufua mashamba pori ya zao la korosho.