Mei 29, 2024 03:24
Bodi ya Korosho Tanzania
Habari ZinazojiriKiteleziMatukio

BODI YA KOROSHO YAZINDUA RASMI MKUTANO WA KIMATAIFA WA KOROSHO 11-13 OCTOBA 2023 JNICC-DAR ES SALAAM

Bodi ya Korosho Tanzania katika kusimamia maendeleo ya Tasnia imeweka malengo makuu matatu ambayo ni: Kuongeza uzalishaji wa korosho ghafi kufikia tani 1,000,000 ifikapo 2030; Kubangua asilimia 60 ya korosho hizo; na Kuwa na masoko ya uhakika na endelevu ya korosho na bidhaa zake ifikapo 2030 ili kufikia agenda 10/30.

Agenda 10/30 inaelekeza sekta ya kilimo kuchangia asilimia 10 ya pato la Taifa na kuingiza fedha za kigeni kwa wingi. Kwa mujbu wa Taarifa ya Hali ya Uchumi ya Mwaka 2022, zao la korosho liliongoza kwa kuliingizia Taifa kiasi cha Dola za Marekani Milioni 226.9 ikilinganishwa na mazao mengine ya tumbaku (USD 178.5M); kahawa (USD 161.2M); pamba (USD 103.4M); karafuu (USD 42.18M); chai (USD 30.0M) na mkonge (USD 24.3M). Aidha ni wazi kuwa fursa zilizoko kwenye Tasnia ya Korosho zikitumika kwa ufanisi Taifa linaweza kujipatia fedha nyingi zaidi za kigeni.

Bodi ya Korosho Tanzania inaandaa Mkutano wa Kimataifa wa Korosho wenye wazo kuu FURSA ZA UWEKEZAJI KWENYE TASNIA YA KOROSHO TANZANIA (AN INSIGHT AND INVESTMENT OPPORTUNITIES IN CASHEW INDUSTRY TANZANIA) na kauli mbiu ni WEKEZA KWENYE KOROSHO KWA MENDELEO ENDELEVU (INVEST IN CASHEW FOR SUSTAINABLE DEVELOPMENT).

Mkutano huu unakusudia kutangaza fursa za uwekezaji zilizoko kwenye Tasnia ya Korosho kuanzia shambani ambapo tunategemea kupata uwekezaji wa kwenye 2 mashamba makubwa, Ubanguaji ambapo matarajio ni kuongezeka kwa viwanda vya kubangua na kusindika korosho na bidhaa zake na kuimarika kwa masoko kwa kufungua masoko ya korosho na bidhaa zake ndani na nje ya nchi.

Kwa upekee Mkutano huu utatumika kuhamasisha matumizi ya korosho na bidhaa zake ndani ya nchi kama vile mafuta ya ganda la korosho (Cashewnut Shell Liquid – CNSL), sharubati (juice), maziwa ya korosho (cashew milk), mvinyo (wine), nyama ya mabibo (cashew apple meat) na pombe kali.

Aidha bidhaa nyingine kama ethanol zinaweza kutumika kwenye maabara za hospitali na shule zetu na hivyo kupanua wigo wa soko la korosho.

Mkutano wa Kimataifa wa Korosho wa Mwaka 2023 unakusudiwa kuhudhuriwa na washiriki 500 kutoka nchi zote Duniani zikiwemo nchi 33 zinazolima korosho. Nchi hizo ni pamoja na Ivory Coast, Cambodia, India, Vietnam, Brazil, Indonesia, Sri Lanka, Nigeria, Guinea Bissau, Burkina Faso, Mali, Benin, Ghana, Madagascar, Zambia, Msumbiji, Kenya, Mauritius, Visiwa vya Komoro na wenyeji Tanzania.

Aidha, mkutano huo utashirikisha wadau mbalimbali kutoka nchi ambazo ni walaji wa korosho ikiwa ni pamoja na Marekani, Nchi za Ulaya, China, Uarabuni, Mashariki ya Kati ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini na nchi zingine za bara la Afrika.

Mkutano unakusudia kuwa na washiriki wote walioko kwenye mnyororo wa thamani wa Tasnia ya Korosho kama vile wakulima, wabanguaji, wasindikaji, wakaangaji, wasafirishaji, Vyama vya Ushirika, Wasambazaji wa pembejeo, waendesha ghala, watafiti, wazalishaji wa mitambo na vipuli, wasimamizi wa Tasnia, walaji au watumiaji wa bidhaa za korosho, Taasisi za fedha, watunga sera, wawekezaji, wabia wa maendeleo na wadau wengine wengi.  

Mkutano wa Kimataifa wa Korosho unatarajiwa kuwa na mada mbalimbali kama vile: Kilimo cha korosho na matumizi ya mashine (Cashew production & Agro[1]mechanisation); Matumizi ya Teknolojia kwenye Tasnia ya Korosho (Technology transfer in cashew value chain);

Fursa za Uwekezaji kwenye Tasnia ya Korosho nchini Tanzania (Investment opportunities in cashew industry in Tanzania); Mfumo wa upatikanaji wa fedha kwenye Tasnia ya Korosho (Financing mechanism in cashew industry); Teknolojia ya Ubanguaji/Usindikaji wa Korosho (Processing technology and techniques);

Matumizi ya soko la korosho na bidhaa zake kwa ujumla (Enhancing marketing of cashew and value-added products globally); Matumizi ya Kidigitali kwenye Tasnia ya Korosho (Digitalization in cashew industry); na Motisha na sera wezeshi kwenye Tasnia ya Korosho (Incentives and fiscal policies in cashew Industry).

Mada hizi zitawasilishwa na Wataalam bobezi na wawekezaji wenye uzoefu kutoka nchi mbalimbali na hivyo kuwezesha washiriki kujifunza kutoka kwao.

Aidha, Kutakuwa na muda wa majadiliano, kubadilisha uzoefu na mawasiliano ili kutengeneza mtandao wa uwekezaji na biashara.

Kupitia mkutano huu tunategemea kuongezeka kwa uwekezaji na biashara kwenye Tasnia ya Korosho hivyo kuwezesha mkulima kupata tija ya zao lake.

Aidha Bodi ya Korosho imeandaa fomu ya kidigitali iliyoko kwenye tovuti ya Bodi ya Korosho Tanzania (www.cashew.go.tz) ambayo itatumiwa na washiriki kuomba kuhudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Korosho wa mwaka 2023. Mshiriki atajaza fomu hii na kuituma ofisi za Bodi ili kufanikisha maandalizi mengine.

Aidha, washiriki wa ndani ya nchi wataweza kupiga namba ya bure ya Bodi 0800112159 ili kupewa maelekezo ya namna ya kujisali pale watakapokuwa na changamoto kwenye kujaza fomu.

Pia kutakuwa na fomu za usajili kwenye ofisi za Bodi zilizoko Mtwara, Dar es 4 Salaam, Tanga Tunduru, Manyoni na Morogoro ambazo mshiriki atajaza na kuziacha hapo ofisini.

Bodi ya Korosho inawasisitizia Watanzania hususani wakulima, wawekezaji na wadau kwa ujumla kutumia fursa hii adhimu kuhudhuria mkutano huu ili kuweza kujifunza kutoka kwa nchi zilizofanikiwa na zaidi katika zao la korosho.

Aidha, mkutano huo ni fursa ya kupata wawekezaji wa kuweza kushirikiana nao katika miradi mbalimbali ya korosho.

Related posts

Wajumbe wakiwa kwenye Mkutano wa kimataifa wa korosho uliofanyika Tanzania katika ukumbi wa Mikutano ya kimataifa wa Julius Nyerere

Peter Luambano

PEMBEJEO BILA MALIPO KWA WAKULIMA

Fesam

NYONGEZA NA. 1 YA MWONGOZO NA. 2 WA USIMAMIZI NA UDHIBITI UBORA WA KOROSHO GHAFI KWA MWAKA 2023/2024

Peter Luambano