Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Ernest Silinde (Mb), amesema kilimo cha korosho sasa kitalimwa katika maeneo ya mikoa mingine kutoka mikoa mitano (5) ya hapo awali hadi kufikia mikoa kumi na nane (18), ili kuongeza juhudi za uzalishaji na kupanua mashamba ya korosho.
Naibu Waziri Silinde amesema hayo tarehe 11 Oktoba 2023, wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Korosho 2023 ulioanza leo nchini katika Ukumbi wa Mikutano ya Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, ambapo amesema katika juhudi za kuongeza uzalishaji, Mikoa hiyo mitano ni Tanga, Mtwara, Lindi, Ruvuma na Pwani.
Amesema katika mikoa inayofikia 18 inayokusudiwa ni pamoja na Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Kigoma, Rukwa, Geita, Manyara, Shinyanga, Iringa, Songwe, Mbeya na Njombe ambapo upanuzi huo utatoa chanzo cha mapato kwa wakulima.
Ameongeza kuwa upanuzi wa kilimo cha Korosho utasaidia utunzaji wa mazingira katika maeneo yenye ukame hapa nchini (climate-smart agriculture).
Mkutano wa Kimataifa wa Korosho 2023 umefunguliwa na Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo washiriki zaidi ya 600 kutoka mataifa zaidi ya 50 wanashiriki. Washiriki hao ni pamoja na watunga sera, wakulima, wafanyabiashara, Taasisi za Serikali na Binafsi, wawekezaji, n.k.