Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amefungua Mkutano wa Kimataifa wa Korosho 2023 leo tarehe 11 Oktoba 2023 katika Ukumbi wa Mikutano ya Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo umehudhuriwa na wadau zaidi ya 600 kutoka mataifa mbalimbali duniani ambapo kauli mbiu ya Mkutano ni Wekeza kwenye Korosho kwa Maendeleo Endelevu.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Dkt. Mpango amesema kuwa korosho ina mchango mkubwa katika uchumi kutokana na fursa zake katika soko la kimataifa ambapo kwa mwaka jana(2022), ilikadiriwa kuwa ni Dola za Marekani bilioni 7.
Amesema Mauzo ya zao hilo yanatarajiwa kukua na kufikia Dola za Marekani bilioni 10.5 kufikia mwaka 2030.
Hivyo, Makamu wa Rais amewataka wadau wa korosho wanaoshiriki Mkutano huo wa Kimataifa kujadiliana na kuandaa mikakati itakayoziwezesha nchi zao ikiwemo Tanzania kunufaika na zao hilo.
Amehamasisha wadau wa wanaoshiriki Mkutano kujadili mbinu za kuongeza thamani ya zao hilo ili kuondoa vikwazo vya tozo mbalimbali gandamizi, kubadilishana uzoefu wa teknolojia zitakazosaidia kuongeza uzalishaji na kuwezesha upatikanaji wa takwimu za zao hilo.
Makamu wa Rais amesema chini ya Mkakati wa Serikali wa kuleta mabadiliko kwenye Sekta ya Kilimo wa Ajenda 10/30 unaotoa mwongozo wa kuongezeka kwa ukuaji wa sekta ya kilimo kutoka asilimia 5 ya sasa hadi 10 kufikia mwaka 2023, zao la korosho ni kati ya mazao ya kimkakati yanayolengwa kuchangia ukuaji huo.
Amesema, kwa miaka kumi sasa, zao la korosho limekuwa kwenye ukuaji wa wastani wa tani 220,000 yani tangu mwaka 2013/2014 na lengo la Serikali ni kufikia mwaka wa 2030 uzalishaji uwe wa tani 1000,000.
Amefafanua dhamira hiyo kwa kuonesha malengo ya kuanzia mwaka wa 2023/2024 ni kufikia tani 400,000 na pia kwa mwaka wa 2026/2027 ifikie tani 700,000