Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Ahmed Abbas Ahmed alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa minada ya korosho kwa msimu wa 2022/2023.
Akihutubia katika halfa hiyo, Mkuu wa Mkoa alivipongeza Vyama vya ushirika kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuhudumia na kusimamia soko la wakulima wa zao la korosho na mazao mengine yanayotumia stakabadhi ghalani.
Pia alikishukuru chama kikuu cha ushirika TANECU kwa kumpa nafasi ya kuhudhuria hafla hiyo ikiwa ni mara yake ya kwanza kushuhudia tukio kubwa na la kihistoria katika kijiji cha Mitondi B.
Katika minada yote miwili iliyofanyika katika vyama vikuu vya, TANECU na MAMCU, jumla ya Tani 8,123 zilipigwa mnada, kati ya hizo, Chama kikuu cha TANECU kikiwa na tani 1,610 na MAMCU tani 6,513 ambapo kwa minada yote miwili wastani wa makampuni 16 yalijitokeza kununua korosho hizo kwa njia ya mnada na bei ya juu kwa minada yote miwili ilikua Sh. 2,011 na bei ya chini ni Sh. 1,630 huku chama kikuu cha MAMCU kikiwa na bei ya juu Sh. 2000 na bei ya chini Sh. 1,830 na Chama kikuu cha TANECU bei ya juu ilikuwa ni Sh. 2011 na bei ya chini Sh. 1,630.
Hata hivyo korosho hizo hazikuweza kuuzwa baada ya wakulima kutokubaliana na bei zilizotolewa na wanunuzi. Korosho hizo sasa zitauzwa katika mnada unaofuata.
Akiongea katika hafla hiyo, wakati wa ufunguzi, Mwenyekiti wa chama kikuu cha TANECU, Bw. Karim Chipola, aliwaeleza wakulima kuwa wao ndio wenye uamuzi wa kuuza au kutokuuza. Hivyo aliwasihi kutumia busara wakati wa kufanya maamuzi.