Jumla ya tani 5,106 za korosho ghafi zimeuzwa kupitia mfumo wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX) katika mnada wa kwanza wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Lindi Mwambao mkoani Lindi, kwa bei ya juu ya shilingi 2,460 na bei ya chini ya shilingi 2,310 kwa kilo.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Francis Alfred amesema mnada huo umefanyika kwa mafanikio makubwa, huku akibainisha kuwa mfumo wa TMX ni mfumo wa uwazi na ushindani katika biashara ya korosho.
Aidha Mkurugenzi ametoa wito kwa wakulima wote kuendelea kuzingatia ubora wa korosho zao kwa kuzikausha vizuri, kwani soko zuri hutegemea ubora wa zao.
Mnada huu umefanyika novemba 9, 2025 ukiwa ni wa pili tangu kuanza kwa minada ya zao la korosho nchini katika msimu wa 2025/2026. Mnada wa kwanza ulifanyika Novemba 8,2025. kupitia Chama Kikuu cha Ushirika Cha Tandahimba na Newala (TANECU).

