Mkuu wa Mkuu wa Mtwara Mhe.Kanali Ahmed Abbas Ahmed azindua rasmi mbio za Korosho Marathon kwa msimu wa pili wa 2023 ikiwa ni mwendelezo wa mbio hizi toka zianzishwe kwa mara ya kwanza na Bodi ya Korosho mwaka 2022,uzinduzi huo uliofanyika 13 Mei,2023 ulitanguliwa na zoezi la ugawaji wa mashine 100 za kubangulia Korosho kwa vikundi vya ubanguaji mbambali Nchi nzima.
Akizungumza katika hafla hiyo ya ugawaji mashine,Kanali Ahmed Abbas amevipongeza vikundi vyote vilivyopatiwa mashine hizo lakini pia ameviaasa kutumia fursa waliyoipata kwa ajili ya kujiletea maendeleo zaidi na kukuza kipato chao.
Vilevile amempongeza mbunifu wa utengenezaji wa mashine za ubanguaji Ndug.Zaidu Mtwana na kuwaomba vijana wengine kuwa na uthubutu wa kujaribu katika kila jambo kuliko kutegemea ubunifu kutoka kwa watu wa nje ili hali uwezo wanao.
Aidha Mhe. Ahmed Abbas alitumia fursa hii pia kuipongeza Bodi ya Korosho kwa ubunifu wa kuchangisha fedha za kusaidia maendeleo kwa jamii inayowazunguka kwa kutumia mbio za marathon na kuiomba Bodi isiishie hapo tu bali iangaze sekta zote ikiwamo Elimu, Afya,Michezo na mambo mengine.
Mbio za marathoni kwa msimu wa pili zitafanyika tarehe 2 Septemba 2023 Mjini Mtwara zikiwa na lengo la kuchangisha fedha kwaajili ya kusaidia sekta ya Elimu kwa msimu huu wa pili.