Disemba 11, 2024 09:05
Bodi ya Korosho Tanzania
Habari ZinazojiriKiteleziMatukio

HALI YA SOKO LA KOROSHO GHAFI KWA MWAKA 2022/2023

Mnamo tarehe 21 Oktoba 2022 minada ya korosho ilianza rasmi; ambapo minada ilifanyika katika vyama vikuu vya TANECU na MAMCU katika eneo la Mitondi B Tandandahimba na Chingulungu Masasi Mtawalia. TANECU bei ya chini ilikuwa shilingi 1,630 na bei ya juu shilingi 2,011. Wakati katika Chama cha MAMCU bei ya chini ilikuwa shilingi 1,800 na bei ya juu shilingi 2,000. Aidha, siku iliyofuata tarehe 22 Oktoba, 2022 mnada ulifanyika chama kikuu cha Lindi Mwambao  katika Halmashauri ya Mtama ambapo bei ya chini ilikuwa shilingi 1,507 na bei ya juu ilikuwa shilingi 1,900. Mnamo tarehe 23 Oktoba, 2022, Mnada ulifanyika Chama Kikuu cha RUNALI Kijiji cha Ndomondo katika Wilaya ya Nachingwea. Katika mnada huo bei ya chini ilikuwa shilingi 1,480 na bei ya juu ilikuwa shilingi 2,200. Katika minada yote iliyofanyika kuanzia tarehe 21 hadi 23 Oktoba, 2022 wakulima walikataa kuuza korosho kutokana na kutoridhika na bei zilizotolewa na wanunuzi

Minada ya Korosho ghafi kwa mwaka 2022/2023 imeonyesha kuwa na mwenendo usioridhisha hasa kutokana na wakulima kutoridhika na bei inayotolewa na wanunuzi. Hali hii imesababisha wakulima kushindwa kuuza korosho zao na mauzo kupelekwa wiki inayofuata, wakati makusanyo ya korosho katika ghala za minada yakiendelea. Serikali kupitia Bodi ya Korosho itaendelea kusimamia minada hiyo na kutoa elimu kwa wakulima juu ya mwenendo wa soko la korosho ulimwenguni. Wakulima wa korosho wataendelea kupewa kipaumbele cha kufanya maamuzi sahihi ya kuuza ama kutokuuza korosho zao bila kulazimishwa na chombo chochote.

Pamoja na Bodi ya korosho kuelezea mwenendo wa biashara ya korosho katika soko la dunia wakati wa minada, bado wakulima wamekuwa wakilalamika kwamba bei zinazotolewa na wanunuzi ziko chini ikilinganishwa na matarajio yao.

Ifamike kwamba uzalishaji wa korosho duniani umekua ukiongezeka kila mwaka huku zaidi ya nchi 20 nyingi zikiwa barani Afrika zikitegemea masoko ya India na Vietnam pekee. Uzalishaji wa Afrika kwa sasa ni tani milioni 2.3 ikilinganishwa na tani 900,000 zilizozalishwa miaka kumi iliyopita. Aidha, Uzalishaji duniani umeongezeka kutoka wastani wa tani 1,400,000 kwa mwaka 2010 hadi kufikia zaidi ya tani 4,100,000 kwa mwaka 2021, hivyo kuna ongezeko kubwa la korosho ghafi duniani. Bara la Afrika linazalisha asilimia 56 ya korosho zote ulimwenguni, huku ubanguaji ukiwa ni chini ya asilimia 10. Hivyo kiasi kikubwa cha korosho ghafi inayozalishwa Afrika, hutegemea soko la India na Vietnam.

Takriban asilimia 90 ya korosho zinazozalishwa ulimwenguni hubanguliwa katika nchi mbili ambazo ni India na Vietnam. Hivyo soko kuu la korosho ghafi ni India na Vietnam.

Tanzania huanza msimu wake wa mauzo mwezi Oktoba, sambamba na nchi za Indonesia, Brazil, Msumbiji, Kenya na Zambia. Msimu huu huanza mara tu baada ya msimu wa mauzo katika nchi za Afrika Magharibi kumalizika ambazo huzalisha kiasi kikubwa cha korosho ghafi Afrika na duniani. Wakati Tanzania inaanza kuuza korosho ghafi msimu wa 2022/2023 bado kulikuwa na bakaa ya korosho katika nchi za Nigeria, Ghana, Benin, Togo na Guinea Bissau; takriban tani 70,000 ambazo zimeendelea kuuzwa sambamba na msimu wa Tanzania.

Kupanda ama kushuka kwa bei ya korosho hutokana na kupungua ama kuongezeka kwa mahitaji/ulaji wa Korosho karanga katika soko la India na Masoko ya China, bara la Ulaya na Marekani ambao ndio walaji wakubwa wa korosho. Hali ya sasa katika soko la India na Vietnam, kuna uwepo wa kiasi kikubwa cha korosho walizonunua kutoka nchi za Afrika Magharibi takribani tani 400,000 ambazo zinaendelea kubanguliwa na kuuzwa taratibu kwa sababu ya kupungua kwa mahitaji ya walaji na hivyo kusababisha baadhi ya viwanda nchini Vietnam kufungwa.

Uwepo wa kiasi kikubwa cha korosho ghafi katika nchi hizo, kina athari ya moja kwa moja ambapo bei zimeshuka katika masoko husika na kuathiri bei ya korosho ghafi katika nchi yetu kwa sasa. Kwa mfano katika nchi za Ivory Cost na Benin kipindi cha msimu bei ya chini ilikuwa n idola 0.61 kwa kilo sawa na Shilingi 1,400; nchini Guinea Bissau bei ya juu ilikuwa dola 0.76 sawa na shilingi 1,748 Aidha, Nchi ya Msumbiji ambao ni Jirani zetu wametangaza kuwa bei katika ngazi ya mkulima (farm gate price) ni dola za kimarekani 0.56 sawa na shilingi 1,288 kwa kilo.

Pamoja na kwamba Tanzania imekuwa ikijivunia kuuza korosho zake kwa bei ya juu ya wastani kutokana na ubora wa korosho zake; Athari, ya mwenendo duni wa soko la korosho ulimwenguni katika mwaka 2022, tayari imejionesha katika baadhi ya minada iliyofanyika hadi sasa.

Hivyo Mwenendo wa bei zisizowaridhisha wakulima katika minada ni kutokana na hali halisi iliyopo katika soko la dunia. Msimu uliopita wa 2021/2022 ambapo tuliuza korosho daraja la kwanza kati ya shilingi 2,445 na shilingi 1,750 kwa kilo katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba, 2021. Katika kipindi hicho cha msimu wa 2021/2022, bei za korosho katika soko la dunia zilikuwa kati ya dola 1,300 hadi 1,600 kwa tani ikilinganishwa bei ya kati 1,080 na 1,280 iliyopo sasa. Bei hizo ni baada mzigo kuwa umenunuliwa na kufika aidha, India au Vietnam (CIF Price).

Kulingana na uhitaji, bei za korosho ghafi zinaweza kupanda au kushuka. Bodi ya Korosho Tanzania inaendelea kufuatilia mwenendo wa bei katika soko la dunia na kutoa taarifa ili wadau wote waweze kufahamu kinachoendelea katika masoko hayo na kufanya maamuzi sahihi katika biashara ya korosho kupitia minada na soko la awali.

Serikali imeendelea na jitihada ili kuongeza ubanguaji wa korosho hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuruhusu uwepo wa soko la awali na kuhamasisha uwekezaji kwenye ubanguaji ambapo  katika msimu huu kuna viwanda vipya sita (6) vyenye uwezo wa kubangua tani 28,600 vimefunguliwa na hivyo kuongeza uwezo wa viwanda kubangua hadi kufikia tani 64,000 za korosho ghafi.

Aidha, hivi karibuni tumefungua soko la Marekani kuuza korosho zilizobanguliwa na kufungashwa katika vikasha/vifungashio kwa ajili ya mlaji (consumer packaged products); upanuzi wa soko hili utachajiza uuzaji wa soko iliyobanguliwa kutoka Tanzania. Pia kumekuwa na ongezeko la uzalishaji wa mafuta ya ganda ya korosho (Cashewnut Shell Liquid – CNSL), ambapo katika msimu uliopita lita 55,000 ziliuzwa nje ya nchi.

Pia, Bodi ya Korosho Tanzania ina mpango wa kujenga kiwanda cha mfano kitakachotumika kwa ajili ya mafunzo na kumalizia uchakataji wa korosho iliyobanguliwa kutoka katika viwanda vingine ambavyo havikidhi viwango ikiwa ni pamoja na korosho kutoka katika vikundi vya ubanguaji na wabanguaji mmoja mmoja.

Hivyo jitihada zaidi zinahitajika miongoni mwa wadau wote kuongeza ubanguaji wa korosho hapa nchini pamoja na uzalishaji wa bidhaa zingine zitokanazo na zao la korosho ili kupanua wigo wa soko la korosho zinazozalishwa hapa nchini-Francis Alfred, Kaimu Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Korosho Tanzania.

Related posts

PEMBEJEO BILA MALIPO KWA WAKULIMA

Fesam

RATIBA YA MINADA KWA MSIMU WA 2023/2024

Peter Luambano

TANGAZO KWA WADAU WOTE WA TASNIA YA KOROSHO NCHINI

Amani Ngoleligwe