Mkuu wa wilaya ya Mtwara Ndg. Abdallah Mwaipaya amefungua mafunzo elekezi ya kuwajengea uwezo maafisa kilimo waliopangiwa vituo vya kazi Wilaya ya Mtwara ikiwa ni moja kati ya vituo tisa vya mafunzo kwa maafisa kilimo vijana 500 walioajiriwa na Bodi ya Korosho Tanzania chini ya programu ya JENGA KESHO ILIYO BORA (BBT) iliyopo Wizara ya Kilimo huku akiwataka kufanya kazi kwa bidii.
Ndugu Mwaipaya amefungua mafunzo hayo tarehe 14 Januari, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Bodi ya Korosho Tanzania mkoani Mtwara ikiwa ni moja kati ya vituo tisa vinavyotoa mafunzo hayo, katika ufunguzi huo Mkuu wa Wilaya amesema kuwa hatua hii ni utekelezaji kwa vitendo ilani ya Chama Cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Dkt. SAMIA SULUHU HASSAN Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika jitihada za kuendeleza zao la korosho nchini kutokana na mchango wake katika kuongeza kipato kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Aidha amesema kuwa lengo kuu la mpango wa kuajiri vijana 500 ni kuongeza uzalishaji wa korosho ghafi nchini kufikia tani 700,000 mwaka 2025/2026 na tani 1,000,000 ifikapo mwaka 2029/2030.
Vilevile ameipongeza Bodi ya Korosho Tanzania kwa usimamizi mzuri wa zao la korosho hapa nchini ambapo kwa mara ya kwanza katika msimu huu wa mwaka 2024/2025 kumeshuhudiwa ongezeko kubwa la uzalishaji wa korosho ghafi kutoka tani 310,787 msimu wa mwaka 2023/2024 hadi kufikia tani 410,000.