Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) ndg. Francis Alfred, leo oktoba 28/2025 amekutana na watumishi wote wa bodi hiyo katika ukumbi wa mikutano wa makao makuu, ambapo amewasisitiza kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29,2025.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu amewataka watumishi wote kutumia haki yao ya kidemokrasia kwa amani, utulivu na uzalendo, akisisitiza kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kuchangia katika mchakato wa kuamua mustakabali wa Taifa.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu amewakumbusha watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na uadilifu, akisema kuwa nidhamu na uwajibikaji ndivyo vinavyojenga taasisi imara na kuongeza tija katika maendeleo ya tasnia ya korosho nchini.
Katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 jumla ya wapiga kura 37,647,235 wanatarajiwa kupiga kura, ambapo kati ya hao, wapiga kura 36,650,932 wapo Tanzania Bara na wapiga kura 996,303 wapo Zanzibar, jumla ya majimbo yote ya Jamhuri ya Muungano ni 272, ambapo kwa Tanzania Bara yapo 222 na Zanzibar yapo 50.

