Madiwani wa Halmashauri ya mji Nanyamba wameeleza kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa Kongani la viwanda vya kubangua korosho lililopo katika Kijiji cha Maranje Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara, mradi ambao upo katika eneo la ekari 1,572.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha taarifa ya maendeleo ya mradi huo, kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania ndg. Mangile Malegesi, amesema kuwa Kongani hili litakuwa na viwanda 30 vya kubangua korosho, Viwanda 6 vya kukamua mafuta ya ganda la korosho, viwanda 4 vya kusindika ufuta, viwanda vya kusindika bidhaa zitokanazo na mabibo ya korosho kama sharubati, mvinyo na pombe kali (ethanol).
Kadhalika mpango uliopo ni kujenga ghala 100 za kuhifadhia mazao ya korosho na ufuta sambamba na huduma mbalimbali kama vile maduka makubwa, nyumba za kuishi wafanyakazi, viwanja vya michezo, migahawa, kituo cha polisi, jeshi la zimamoto na uokoaji, kituo cha kutoa huduma kwa wawekezaji na nyingine nyingi.
Kwa upande wake Mhandisi Daudi Ndabachahe wakati akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa mradi huo amesema kuwa kwasasa wanaendelea na ujenzi wa barabara na ghala katika kongani hilo na hakuna changamoto yoyote inayokwamisha kasi ya ujenzi.
Makadirio ya gharama za mradi wa kongani la viwanda ni dola za Kimarekani 127,189,692.00 ambazo ni sawa na shilingi za Kitanzania 343,412,168,260.00 ambapo baadhi ya gharama hizo zitalipwa na serikali na nyingine zitakuwa za wawekezaji.
Mradi huu ambao ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa akiwa kwenye ziara katika mikoa ya Mtwara na Lindi mwezi septemba 2023 unatarajiwa kukamilika ndani ya muda wa miaka mitano kuanzia 2023 hadi 2027.