Disemba 12, 2025 07:01
Bodi ya Korosho Tanzania
Habari ZinazojiriKiteleziMatukio

SERIKALI YALETA NEEMA KWA WAKULIMA WA KOROSHO


Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb) amefanya ziara ya kikazi mkoani Mtwara tarehe 11 Desemba 2025 na kutoa salamu za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa “Serikali itaendelea kuwapunguzia mzigo wakulima wa Korosho kwa kuwa na uhakika wa pembejeo za kilimo.”

Waziri Chongolo ameongeza kuwa Serikali itahakikisha Korosho zote ghafi zinazosafirishwa zitumie Bandari ya Mtwara ili manufaa na maslahi yanayohusisha mchakato wa Korosho yanaacha neema katika mikoa ya kusini.

Akitoa maelekezo kwa Bodi ya Korosho Tanzania, Waziri Chongolo amesisitiza Bodi hiyo kuendelea kulinda soko la awali la Korosho ili kukabiliana na walanguzi holela (maarufu kama kangomba).

Waziri Chongolo ametembelea pia Kongani ya Viwanda iliyopo Maranje ambayo inalenga kuwa na viwanda vya kubangua Korosho ili kuwezesha wakulima kupata tija na thamani zaidi kwenye zao hilo.

Waziri Chongolo pia amesisitiza kuwa kiwanda hicho kiwe na maabara ya kisasa kupima unyevu wa Korosho ili kuhakikisha Korosho zinakuwa bora na shindanishi katika soko la Kimataifa hususan China na Vietnam.

Aidha, Waziri Chongolo amekagua Kituo cha Tafiti za Kilimo cha TARI – Naliendele, na kuwataka watafiti wake kuongeza thamani za ubora wa mbegu na kupunguza visumbufu kwa kuhuisha teknolojia na sayansi katika zao la Korosho, akitolea mfano unyunywizaji wa dawa ya viuwadudu (Sulphur) kwa kutumia teknolojia ya ndege nyuki (drone).

Related posts

MAMCU WAUZA KILO 35,445,155 KWA BEI YA JUU SH. 2,510

Amani Ngoleligwe

TANGAZO LA MKUTANO WA WADAU 2025

Amani Ngoleligwe

KIKAO NA MTANDAO WA WAKULIMA WA KOROSHO TANZANIA

Amani Ngoleligwe