Waziri wa kilimo nchini, Mhe. Hussein Bashe ameeleza manufaa ya TOZO YA USAFIRISHAJI WA ZAO LA KOROSHO GHAFI NJE YA NCHI (EXPORT LEVY) kutumika kwa wakulima kwani awali tozo hii ilikuwa ikienda kwenye mfuko mkuu wa Hazina.
Amesema kuwa manufaa hayo ni pamoja na kununua viuatilifu kwa ajili ya wakulima wa korosho, kuajiri maafisa ugani, kununua vitendea kazi kama vile pikipiki, vishikwambi pamoja na mambo mengine ili kuwanufaisha wakulima wa Korosho.
Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu kwa moyo wa dhati matumizi ya Export Levy katika Tasnia ya korosho nchini.
Waziri Bashe ameyasema hayo Aprili 30, 2025 katika ukumbi wa PSSF jijini Dodoma wakati wa kikao cha Tathmini ya Uzalishaji, Ubanguaji na Masoko ya Korosho msimu wa 2024/2025 na Mipango ya Msimu wa 2025/2026.
Kikao hicho kimefanyika jijini Dodoma kikiwakutanisha viongozi wa Bodi ya Korosho Tanzania, wafanyakazi, wadau wa Tasnia ya Korosho, viongozi wa Chama na Serikali huku Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe akiwa ni mgeni rasmi wa kikao hicho.