Novemba 27, 2025 02:47
Bodi ya Korosho Tanzania
Habari ZinazojiriKiteleziMatukio

TPAWU TAWI LA BODI YA KOROSHO TANZANIA WACHAGUA VIONGOZI WAPYA

Wanachama wa chama cha wafanyakazi wa sekta ya Kilimo na Mashamba TANZANIA PLANTATION AND AGRICULTURAL WORKERS UNION (TPAWU) wamefanya uchaguzi Mkuu wa Viongozi wa Tawi la Bodi ya Korosho Tanzania katika ngazi ya Mwenyekiti, Katibu, Wajumbe wa Kamati ya Utendaji, Kamati ya wanawake na Kamati ya vijana.

Kwa upande wa nafasi ya Mwenyekiti, ndugu. Andambike Emmanuel Mwakilema ameibuka mshindi kwa kura 18 dhidi ya Azalia Sanga aliyepata kura 7, Liberatus Soka ameibuka mshindi kwa nafasi ya Katibu wa Tawi kwa kupata kura 24 za ndio na 1 ya Hapana.

Aidha wajumbe wa Kamati ya Utendaji waliochaguliwa ni ndugu. Omary Kavanga, Angelina Boaz, Salama Wakati, Allan Mrope, Winifrida Kasagula na Mahara A. Mahara. Hao wote wamepita kwa kura 25 za ndio bila kupingwa na yeyote.

Wakizungumza mara baada ya uchaguzi huo, Mwenyekiti Mwakilema na Katibu Soka wamewashukuru Wajumbe kwa kuwaamini kuwapa nafasi hizo na kuahidi kuwa wapo tayari kwa majukumu hayo mapya katika kutengeza mazingira mazuri kwa wafanyakazi ambayo hatimaye yataleta ufanisi mkubwa  na tija katika maendeleo ya Taasisi na Tasnia kwa ujumla.

Awali akimkaribisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu kufungua mkutano huo, Mwenyekiti mstaafu ndugu Christopher Anthony Mwaya ambaye amehudumu katika nafasi hiyo kwa vipindi viwili mfululizo, amesema kuwa katika kipindi cha uongozi wao, kamati ya uongozi ya TPAWU wamejitahidi kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi kwa kushirikiana na Uongozi wa Taasisi kwa njia ya majadiliano na hatimaye kumaliza uongozi wao pasipo kuwepo kwa migorogoro baina ya TPAWU na Menejimenti ya Bodi ya Korosho Tanzania.

Mwaya amewaasa viongozi wapya wa TPAWU kuwa na mahusiano mazuri baina yao na menejimenti ikiwa ni Pamoja na kujenga utaratibu wa kukutana na menejimenti ili kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi kwa lengo la kudumisha mazingira ya utulivu na mshikamano katika Taasisi. Aliendelea kusisitiza kuwa Chama cha Wafanyakazi katika sehemu ya kazi na uongozi wa Taasisi wote wanajenga nyumba moja na hivyo hakuna sababu ya kugombea fito.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mohamed Muhidini, amesema kuwa chama Cha wafanyakazi ni muhimu sana katika eneo la kazi katika kutengeneza mazingira mazuri kati ya mwajiri na wafanyakazi ili kuleta ufanisi katika kazi. Amewataka viongozi hao kuyatafutia ufumbuzi matatizo yote yanayowakabili wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kuyaleta kwenye vikao vya menejimenti.

Related posts

Wajumbe wakiwa kwenye Mkutano wa kimataifa wa korosho uliofanyika Tanzania katika ukumbi wa Mikutano ya kimataifa wa Julius Nyerere

Peter Luambano

AUCTIONS TIME TABLE FOR THE SEASON 2022-2023

Peter Luambano

RAIS DKT. SAMIA KUZINDUA BENKI YA USHIRIKA NCHINI

Amani Ngoleligwe