Imeelezwa kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani, unaotumiwa na wakulima wa zao la korosho, mbaazi na ufuta nchini ni wenye tija na unalenga kumnufaisha mkulima na jamii kwa ujumla ikiwemo kutoa ajira.
Hayo yamesemwa na viongozi wa vyama vikuu vya ushirika vya TANECU, MAMCU NA TAMCU walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari mkoani Mtwara ikiwa ni katika kutoa ufafanuzi juu ya upotoshwaji unaoenezwa na baadhi ya vyama vya siasa nchini kuhusu mfumo huo.
Karim Chipola ambaye ni mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha TANECU kinachosimamia wakulima wa wilaya zaTandahimba na Newala anasema kuwa mfumo huu umewawezesha wakulima kudhibiti uuzaji holela, huwawezesha wakulima kuamua watauza kwa bei gani Pamoja na kupata takwimu sahihi za mazao yao.
Pia kwa upande wake mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha MAMCU, Alhaj Azam Mfaume amewashauri wakulima kutoyumbishwa na maneno ya wanasiasa kwani hata wao ni mashuhuda wa mifumo mizuri ya sasa ya mauzo na malipo kwa wakulima, tofauti na ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.
Naye ndugu Mussa Manjaule, mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika cha TAMCU, ameeleza kuwa Ushirika ni taasisi inayotambulika kisheria, ikisimamia mazao yote ya wakulima yaliyopo kwenye mnyororo wa thamani yakiwamo korosho, ufuta na mbaazi.
Pamoja na mengine mengi, viongozi hao wamewakumbusha wakulima wa zao la korosho ambao bado hawajahuisha taarifa zao, kuhakikisha kuwa wanakwenda kuhuisha taarifa zao katika ofisi za watendaji wa vijiji yalipo mashamba yao, zoezi ambalo linasimamiwa na maafisa kilimo walioajiliwa na Bodi ya Korosho Tanzania chini ya mpango wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) sambamba na viongozi wa vijiji hivyo.