Mkuu wa mkoa wa Lindi Bi. Zainab Telack ametoa wito kwa maafisa kilimo kuendelea kutoa elimu kwa wakulima wa zao la korosho ili kufikia lengo la uzalishaji wa tani 700,000 msimu wa 2025/2026.
Vilevile amewataka vijana mkoani humo kuchangamkia fursa zilizopo kupitia zao la Korosho, pia wakulima na wataalam kuendelea kutunza na kuongeza mashamba ya zao hilo kwani mkoa huo unayo ardhi ya kutosha kwa ajili ya uzalishaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Ndg. Francis Alfred, amesema kuwa mojawapo ya juhudi kubwa ambazo zimefanywa na Bodi ya Korosho Tanzania ni kuendeleza mashamba makubwa ya Korosho ikiwa ni Pamoja na shamba la Manispaa ya Lindi lijulikanalo kama TARUCHINA.
Pia Ndg. Alfred amesema kuwa, iwapo kuna mkulima ambaye wakati wa uhuishaji wa taarifa za wakulima hakuwepo na viongozi wa serikali wamethibitisha kuwa ni mkulima, basi atoe taarifa kwa maafisa kilimo wa BBT na wao wataenda kukagua shamba la huyo mkulima na kisha kuhuisha taarifa zake ili wakulima wote waweze kupata pembejeo za ruzuku zinazotolewa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hayo yanajiri wakati wa kikao cha wadau mbalimbali kujadili kuhusu zao la korosho katika mkoa wa Lindi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.