Wadau mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa zao la korosho wakiwemo Katibu Tawala Wasaidizi Uchumi na Uzalishaji, Warajisi wa Mikoa, Wenyeviti na Meneja wa Vyama Vikuu vya Ushirika, Maafisa Mapato kutoka Halmashauri, Wabanguaji, Wanunuzi, Wasafirishaji na Waendesha ghala kutoka mikoa saba (7) nchini, wamekutana mkoani Mtwara ili kuipitia miongozo kwa msimu wa 2025/2026 na kutoa maoni ya kuboresha miongozo hiyo.
Wadau hao kutoka mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani, Tanga, Singida na Morogoro wanashiriki kikao cha siku mbili (2) kuanzia 17 Julai hadi Julai 18 – 2025, kujadili na kutoa mapendekezo katika rasimu ya mwongozo wa mauzo ya korosho ghafi kupitia Soko la Awali kwa msimu wa 2025/2026, rasimu ya Mwongozo Na.1 wa Usimamizi wa Masoko na Mauzo ya Korosho ghafi kwa msimu wa 2025/2026 na rasimu ya Mwongozo Na. 2 wa Usimamizi na Udhibiti Ubora wa Korosho ghafi msimu wa 2025/2026.
Aidha, katika siku ya kwanza, wadau hao wamejadili na kutoa mapendekezo yao katika rasimu zote tatu (3) za miongozo iliyowasilishwa.
Siku ya pili ya kikao hicho ambayo ni tarehe 18 Julai 2025, inatarajiwa kutumika kufanya majumuisho ya maoni mbalimbali yaliyotolewa na wadau hao kwa lengo la kutoa miongozo kamili iliyojengwa katika misingi shirikishi na ya kisheria.
Kikao cha leo kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Bodi ya Korosho Tanzania mkoani Mtwara, kikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu ndugu Reuben Putaputa.