Tanzania ni mojawapo ya nchi zinazoongoza kwa uzalishaji wa zao la korosho duniani, ikishika nafasi ya pili katika bara la Afrika na nafasi ya sita duniani. Katika msimu wa 2024/2025 uzalishaji wa korosho ulikuwa Tani 528,262.23.
Katika kuhakikisha uzalishaji wa zao hili unafikia tani 700,000 msimu wa 2025/2026 na tani 1,000,000 ifikapo 2030 ikiwa ni jitihada za kuongeza mchango wa zao hili kufikia agenda ya 10/30; serikali imeajiri vijana 500 wa BBT ambao tayari wamesambazwa katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani na Tanga.
Kwasasa zoezi la uhuishaji taarifa za wakulima wa korosho linaendelea kwa mafanikio makubwa katika ofisi za vijiji yalipo mashamba ya wakulima, likiwa chini ya usimamizi wa Maafisa Kilimo walioajiriwa na Bodi ya Korosho Tanzania chini ya mpango wa Jenga Kesho Iliyo Bora (Building a Better Tommorow – BBT) na viongozi wa vijiji husika.
Devotha Ngahi, mkazi wa Kijiji cha Nyangao B kata ya Nyangao ambaye tayari amehuisha taarifa zake anasema kuwa zoezi linaenda vizuri na matarajio yake ni kupata mavuno zaidi ya msimu uliopita.
Naye Mohamed Hassan Mteka, mkulima kutoka katika Kijiji hicho ambaye tayari amehuisha taarifa zake, anasema kuwa katika msimu uliopita amevuna korosho kiasi cha tani tatu na matarajio yake kwa msimu huuu ni kuvuna mara mbili zaidi.
Kata ya Nyangao ina maafisa kilimo wa BBT wapatao wawili ambao wanasimamia shughuli za kilimo cha korosho katika kata hiyo: Bakari Rashid Kambona ambaye ni afisa kilimo wa BBT, anasema kuwa hadi kufikia alhamisi ya tarehe 27/03/2025 walikuwa wamefanikiwa kuhuisha taarifa za jumla ya wakulima 1175 na lengo lao ni kuwahudumia wakulima wapatao 1500.
Naye Bi. Tushabe Joseph Deogratius afisa kilimo wa BBT, aliyepo katika kata hiyo, anaeleza kuwa mwitikio wa wakulima umekuwa mkubwa pia wenye mafanikio, na katika kufanikisha zoezi hili wakati mwingine hulazimika kuwafikia wakulima katika vijiji vyao na kuwahudumia.
Zoezi la uhuishaji taarifa za wakulima wa zao Korosho linafanyika kila siku za jumatatu hadi Jumamosi katika ofisi za watendaji wa vijiji yalipo mashamba ya wakulima kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni. Lilianza rasmi februari 17-2025 na linatarajia kufikia tamati machi 31, 2025.