Skip to main content
WATAFITI KUTOKA KENYA WATEMBELEA BODI YA KOROSHO TANZANIA KUJIFUNZA USIMAMIZI WA TASNIA YA KOROSHO
30 Jul, 2026
admin
Habari na Matukio

WATAFITI KUTOKA KENYA WATEMBELEA BODI YA KOROSHO TANZANIA KUJIFUNZA USIMAMIZI WA TASNIA YA KOROSHO

Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Julai 30, 2026 imepokea ujumbe wa watafiti tisa (9) kutoka nchini Kenya waliotembelea Tanzania kwa lengo la kujifunza mfumo wa usimamizi na maendeleo ya tasnia ya korosho. 

Ziara hiyo imeandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) kupitia mradi wa Market-Oriented Value Chains for Jobs and Growth, unaotekelezwa kwa ushirikiano na taasisi za utafiti kutoka Tanzania na Kenya pamoja na ufadhili wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani (GIZ).

Katika ziara hiyo, wageni hao kutoka Taasisi ya Utafiti wa Misitu Kenya (KEFRI) na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya (KALRO) walipata fursa ya kujifunza kuhusu majukumu ya Bodi ya Korosho Tanzania katika kuratibu, kusimamia na kuendeleza tasnia ya korosho, ikiwemo utekelezaji wa sera, mifumo ya masoko, huduma za ugani pamoja na mikakati ya kuongeza tija na thamani ya zao hilo.

Aidha, ujumbe huo ulijadiliana na wataalamu wa CBT kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika kuimarisha uzalishaji wa korosho nchini kupitia usambazaji wa pembejeo za ruzuku, uboreshaji wa ubora wa korosho, pamoja na uwekezaji katika ubanguaji wa korosho unaolenga kuongeza thamani na kufungua fursa zaidi za ajira na biashara.

Ziara hiyo itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda kati ya Tanzania na Kenya katika nyanja za utafiti, ubadilishanaji wa uzoefu na maendeleo ya mnyororo wa thamani wa zao la korosho. Kupitia ushirikiano huo, pande zote zinatarajia kujifunza mbinu bora zitakazochochea ukuaji endelevu wa tasnia ya korosho na kuongeza manufaa kwa wakulima na wadau wengine wa tasnia.

Pia unaweza kutufuatilia kupitia kurasa zetu za mitandao ya kijamii, Instagram na Threads ni @Cashewnutboard, Facebook, LinkedIn na X ni #Cashewnut Board of Tanzania, Youtube ni Cashewnut Boardtz na Tovuti ni www.cashew.go.tz

Lebo: