KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA VIWANDA, BIASHARA, KILIMO NA MIFUGO YATEMBELEA BANDA LA CBT MAONESHO YA NANENANE
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mheshimiwa Deo Mwanyika, agosti 7,2026 imetembelea banda la Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Maonesho vya John Malecela, jijini Dodoma.
Wajumbe wa kamati walipata fursa ya kujionea bidhaa mbalimbali zinazotokana na zao la korosho zilizoongezwa thamani, pamoja na kupata maelezo kuhusu shughuli zinazotekelezwa na CBT katika kuendeleza uzalishaji, ubanguaji, masoko na kuongeza thamani ya zao hilo nchini.
Aidha, wataalam wa CBT waliieleza kamati kuhusu juhudi zinazoendelea za kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika kilimo cha korosho, utoaji wa elimu kwa wadau wa tasnia pamoja na utekelezaji wa mikakati mbalimbali inayolenga kuongeza tija, ubora wa korosho na mchango wa zao hilo katika uchumi wa Taifa.
Ziara hiyo iliipa Kamati nafasi ya kujionea mafanikio yaliyofikiwa na tasnia ya korosho, fursa zilizopo na hatua zinazoendelea kuchukuliwa ili kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa wazalishaji na wabanguaji wakubwa wa korosho duniani.