Skip to main content
MWENYEKITI WA CBT AWATAKA WAKULIMA KUTUMIA VIUATILIFU VYA MAJI ILI KUONGEZA TIJA KATIKA UZALISHAJI
03 Aug, 2026
admin
Habari Zinazojiri

MWENYEKITI WA CBT AWATAKA WAKULIMA KUTUMIA VIUATILIFU VYA MAJI ILI KUONGEZA TIJA KATIKA UZALISHAJI

Lindi

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Brig. Gen. (Mstaafu) Aloyce D. Mwanjile, ndc, amewataka wakulima wa korosho nchini kutumia viuatilifu vya maji kwa usahihi na kwa wakati ili kudhibiti magonjwa na wadudu waharibifu wa mikorosho, hatua ambayo itachangia kuongeza tija ya uzalishaji, kuboresha ubora wa korosho na kuongeza kipato cha mkulima.

Akizungumza katika Banda la Bodi ya Korosho Tanzania wakati wa Maonesho ya Nane Nane 2026 Kanda ya Kusini yanayoendelea katika Viwanja vya Ngongo, mkoani Lindi, Brig. Gen. Mwanjile alisema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa kuhakikisha viuatilifu vya maji vinapatikana kwa wakulima ili kuwawezesha kuzalisha korosho zenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.

Ameeleza kuwa matumizi ya viuatilifu hivyo yanapaswa kuambatana na kufuata ushauri wa wataalamu wa kilimo pamoja na maelekezo ya matumizi ili kuongeza ufanisi katika kudhibiti magonjwa na wadudu waharibifu wa mikorosho. Aidha, amewahimiza wakulima kuendelea kutumia mbinu bora za kilimo katika hatua zote za uzalishaji ili kuongeza mavuno na thamani ya zao la korosho.

Pia amewataka wakulima, wadau wa tasnia ya korosho na wananchi kutembelea Banda la Bodi ya Korosho Tanzania katika Maonesho ya Nane Nane ili kujifunza kuhusu huduma, teknolojia na fursa mbalimbali zinazotolewa na CBT. 

Lebo: