MKURUGENZI MKUU CBT ASIKILIZA KERO ZA WAKULIMA TANDAHIMBA, MASUALA YA PEMBEJEO, BEI NA UBORA YAPEWA KIPAUMBELE
TANDAHIMBA
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Francis Alfred, amekutana na wakulima wa korosho katika Kata ya Mihambwe, Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara, na kusikiliza maoni, changamoto na mapendekezo yao kuhusu namna ya kuboresha uzalishaji na kuongeza maslahi ya mkulima.
Ziara hiyo iliyofanyika Septemba 9, 2026, ilikuwa sehemu ya programu maalum ya “Kijiwe cha Mkurugenzi Mkuu na Wakulima”, inayolenga kuwapa wakulima na wadau wa Tasnia ya korosho nafasi ya kueleza moja kwa moja changamoto zinazowakabili na kupata ufafanuzi kutoka kwa uongozi wa CBT.
Mkulima Awadhi Saidi ameipongeza CBT kwa kuwaweka Maafisa Kilimo wa BBT katika maeneo ya wakulima, akisema wamekuwa wakifanya kazi vizuri, huku akiomba wapewe nafasi kubwa zaidi katika usimamizi wa pembejeo ili kuhakikisha zinawafikia walengwa na kutumika ipasavyo.
Kwa upande wake, mkulima kutoka Kata ya Mihambwe, Mubarack Fakihi, ameishauri CBT kuhakikisha usimamizi na ugawaji wa pembejeo unafanywa na watu wenye taaluma na uwezo unaohitajika, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza ufanisi na kuondoa changamoto zinazoweza kujitokeza katika mchakato wa ugawaji wa pembejeo.
Naye mkulima Selemani Mshamu ameiomba CBT kuangalia suala la tofauti za bei katika maeneo ya uzalishaji, akieleza kuwa wakati mwingine wakulima wa Tandahimba hupata bei wanayoona kuwa ni ya chini ikilinganishwa na maeneo mengine kama Newala. Ameomba kuwepo kwa utaratibu unaozingatia ubora wa korosho na kuhakikisha mkulima anapata thamani inayostahili kwa mazao yake.
Akijibu hoja hizo, Mkurugenzi Mkuu Francis Alfred amewataka wakulima kuendelea kusimamia ubora wa korosho kuanzia shambani hadi hatua ya uuzaji, akisisitiza umuhimu wa kuzikausha vizuri na kuhakikisha hazina unyevu.
Mkurugenzi Mkuu amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya CBT, wakulima, Maafisa Kilimo na wadau wengine wa tasnia ni muhimu katika kuhakikisha changamoto zinazowakabili wakulima zinapatiwa ufumbuzi na zao la korosho linaendelea kuwa chanzo cha kipato, ajira na maendeleo kwa wananchi.