MAKAMU WA RAIS AWEKA JIWE LA MSINGI LA KONGANI YA VIWANDA MARANJE, AKABIDHI MASHINE 100 ZA KUBANGUA KOROSHO
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Deogratius John Ndejembi, ameweka jiwe la msingi katika Kongani ya Viwanda ya Maranje mkoani Mtwara, ikiwa ni hatua muhimu katika utekelezaji wa mradi huo unaolenga kuongeza thamani ya mazao ya kilimo nchini, hususan zao la korosho. Mradi huo unatarajiwa kuimarisha shughuli za ubanguaji wa korosho, kuvutia uwekezaji, kukuza viwanda vya ndani na kupanua fursa za kiuchumi kupitia uongezaji thamani wa mazao.
Aidha, katika hafla hiyo, Makamu wa Rais amekabidhi jumla ya mashine 100 za kubangua korosho zinazotumia nishati ya umeme, kwa lengo la kuimarisha uwezo wa ubanguaji wa korosho nchini, kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa korosho zilizobanguliwa na kuchochea ukuaji wa viwanda vya ndani.
Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha mnyororo wa thamani wa zao la korosho kwa kuhakikisha sehemu kubwa ya korosho zinazozalishwa nchini zinachakatwa hapa nchini kabla ya kufikishwa katika masoko ya ndani na nje ya nchi. Kupitia uchakataji huo, nchi itanufaika zaidi na bidhaa zinazotokana na korosho badala ya kutegemea zaidi mauzo ya korosho ghafi.
Uwepo wa Kongani ya Viwanda ya Maranje unatarajiwa kufungua fursa zaidi za uwekezaji, kuongeza ajira kwa vijana na wananchi wengine, pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika mikoa ya kusini na taifa kwa ujumla. Aidha, uwekezaji katika miundombinu ya viwanda na teknolojia ya kisasa ya ubanguaji unatarajiwa kuongeza ushindani wa bidhaa za korosho za Tanzania katika masoko ya ndani na kimataifa.