
CBT YATENGA ZAIDI YA MIL. 200 KUIMARISHA HUDUMA ZA UGANI
Bodi ya
Korosho Tanzania (CBT) imetenga zaidi ya shilingi milioni 200 kwa ajili ya
kuendesha mpango wa kuimarisha huduma za ugani utakaotekelezwa kwa awamu ya
kwanza katika mikoa ya Mtwara, Ruvuma, Lindi na Pwani.
Kulingana na
taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo Bwn. Francis Alfred amesema mpango huo
ni kiungo muhimu katika kuwafikishia wakulima ujuzi na teknolojia mbalimbali
zinazogunduliwa na watafiti ili kutatua vikwazo vinavyokwamisha kuongezeka kwa
kiwango cha uzalishaji na tija.
Amesema
katika utekelezaji wa mpango huo, Bodi ya Korosho itashirikiana na Sekretarieti
za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuhakikisha huduma za ugani
zinawafikia wakulima kupitia maafisa ugani.
Hatua hiyo inatokana
na lengo la kuongeza uzalishaji wa korosho ghafi kufikia tani 700,000 ifikapo
mwaka 2025/2026.